Wednesday, April 29, 2009

Taarifa ya Serikali Kuhusu Ugonjwa wa Mafua ya Nguruwe

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii

Tarehe 28 Aprili 2009

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UGONJWA WA MAFUA YA NGURUWE
(SWINE INFLUENZA/FLU)


Chanzo: Michuzi Blog
Utangulizi
Mafua ya Nguruwe ni ugonjwa wa njia ya hewa kwa nguruwe unaosababishwa na virusi (type A influenza viruses) ambavyo mara nyingi husababisha mlipuko wa ugonjwa huo kwa nguruwe.
Kwa kawaida watu hawapati ugonjwa huo wa mafua ya nguruwe lakini maambukizi kwa binadamu huwa yanatokea. Hata hivyo ilishawahi kuripotiwa kuwepo kwa maambukizi kwa binadamu kati ya mtu na mtu.

Nchi ambazo ugonjwa huu umeripotiwa
Kuanzia mwezi Machi mwaka huu hadi sasa, nchi 8 zilizotoa ripoti ya ugonjwa huu kama ifuatavyo: Mexico – wagonjwa 1,614 (suspected and confirmed) na vifo 106; Marekani – wagonjwa 20 (confirmed); Canada - wagonjwa 6; New Zealand – wagonjwa 13 (suspected); Spain – wagonjwa 7 (suspected); France – mgonjwa 1 (suspected); Israel – mgonjwa 1 (suspected); na Brazil – mgonjwa 1 (suspected).

Mafua ya Nguruwe yanavyoambukizwa
Katika wanyama, kati ya nguruwe na nguruwe ugonjwa huo unaambukiza kwa wanyama kuwa karibu na pia kugusana na kitu chenye virusi vya ugonjwa huo. Aidha ugonjwa huo unaweza kuambukiza kati ya nguruwe kwa nguruwe, nguruwe kwa binadamu, binadamu kwa nguruwe, na binadamu kwa binadamu.

Dalili za ugonjwa huu kwa binadamu
Dalili za ugonjwa wa mafua ya nguruwe kwa binadamu ni sawa na dalili za mafua ya kawaida kwa binadamu pamoja na homa, kukohoa, maumivu ya koo, kukosa hamu ya chakula, maumivu ya mwili, kuumwa kichwa, kutetemeka baridi na mwili kuchoka. Kwa baadhi ya watu huharisha na kutapika. Aidha wagonjwa wengine huzidiwa na kupata vichomi (pneumonia), kushindwa kupumua na kusababisha kifo.

Dalili za ugonjwa huu kwa nguruwe
Dalili za ugonjwa kwa nguruwe ni kama ifuatavyo: Homa ya ghafla, mfadhaiko/kuzubaa, kukohoa, mafua, kupiga chafya, kupumua kwa shida, macho kuwa mekundu, na kukataa kula.

Jinsi virusi vya mafua ya nguruwe vinavyoenea kwa binadamu
Ugonjwa unaweza kuambukiza kati nguruwe na bindamu kwa kuwa karibu au kumgusa nguruwe mwenye ugonjwa.

Virusi huenea kutoka kwa mtu kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa kwa kukohoa na kupiga chafya; kugusa kitu chenye virusi hivyo na kujigusa mdomo au pua.

Mtu mwenye ugonjwa huo anaweza kuambukiza wengine siku moja kabla ya dalili za ugonjwa kujitokeza hadi siku saba (7) au zaidi baada ya kuwa mgonjwa. Kwa hiyo mtu anaweza kumwambukiza mwingine kabla ya yeye kujua kama anaumwa na wakati akiwa mgonjwa

Je unaweza kupata ugonjwa wa mafua ya nguruwe kwa kula nyama ya nguruwe?
Huwezi kupata ugonjwa wa mafua ya nguruwe kwa kula nyama ya nguruwe iliyotayarishwa na kupikwa vizuri (nyuzo joto 100 centigrade). Hata hivyo inatakiwa kuchukua tahadhari wakati wa maandalizi kabla nyama haijapikwa.


Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa mafua ya nguruwe

  • Kitu muhimu cha kwanza ni Kunawa mikono vizuri kwa sabuni na maji mara kwa mara
  • Kuepuka kuwa karibu na watu wanaonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo
  • Zuia mdomo na pua kwa kitambaa au karatasi laini wakati unapokohoa au kupiga chafya
  • Kuepuka kushika macho, pua na mdomo
  • Kufuata kanuni za afya bora kwa mfano kufanya mazoezi ya viungo, kupumzika vizuri, kula chakula bora, n.k.

Jinsi ya kutambua na kuthibitisha ugonjwa wa mafua ya nguruwe
Baada ya mtu kuhisihiwa kuwa na ugonjwa, sampuli huweza kuchukuliwa na kuthibitisha katika maabara maalumu. Hapa nchini maabara hiyo ipo katika jengo la Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR/National Influenza Centre).

Tanzania tumejenga uwezo wa kuyatambua magonjwa kama haya hapa nchini baada ya kuwepo maabara za kisasa za kufanyia uchunguzi.


Tiba ya ugonjwa huu
Ugonjwa wa mafua ya nguruwe unatibika na kuzuia kwa dawa aina ya Tamiflu au Zanamivir. Hakuna chanjo kwa binadamu.

Tunawasiliana na Shirika la Afya Duniani hapa nchini ili tuweze kupata dawa za kudhibiti ugonjwa huu.

Hatua zinazochukuliwa na Wizara

  • Kutekeleza mikakati ya kuimarisha ufuatiliaji hasa katika viwanja vya ndege na vituo vya mipakani
  • Kushirikisha wadau husika katika kuchukua tahadhari pamoja na kuzuia kuingia kwa ugonjwa
  • Kuwasiliana na mikoa pamoja na wilaya kuchukua tahadhari
  • Vifaa kinga vipo vya kutosha kwa makundi maalumu ambayo yatahusika kwa karibu iwapo ugonjwa unatokea

No comments:

Post a Comment